Ushuhuda Asha 

Aliolewa akiwa na miaka 13

Mimi naitwa Asha, niliolewa nikiwa na miaka 13 baada ya kumaliza darasa la saba. Nilifaulu kuingia kidato cha Kwanza lakini nilikatishwa masomo na kuolewa na mama zangu wadogo kiukoo ambao walipewa dhamana ya kunitunza baada ya wazazi kuhama hilo eneo mara tu ya mimi kufaulu.

 

Mama wadogo hao walinikataza kwenda shule, wakawa wanaleta wanaume hapo nyumbani wakubwa na wazee. Walikuwa wakinisimanga, kunisema vibaya na kunifanyisha kazi, wakisema niolewe na huyo mwanaume atanitunza na kunisomesha.

 

Niliolewa na kuacha shule na ndipo mateso ya vipigo yalipoanza, yule mwanaume hakuniedeleza ila alikuwa akilewa na kunitukana na kunipiga kwa kosa dogo tu. Akinipiga nilikuwa nakimbilia nyumbani kwa mama wadogo wananifukuza na kunipiga tena. Nilibeba ujauzito lakini bado aliedelea kuninyanyasa na kunipiga. Siku moja alinipiga akaniumiza sana nilikimbilia kwa mama wadogo nao wakanionea huruma hawakunirudisha tena kwa huyo mwanaume. Nilisikia wazazi wangu wamerudi wamehamia kwenye maeneo ya karibu. Nilitoroka nikawafuata, wakashangaa kwamba siko shule. Walikwenda kuripoti polisi. Wale mama wadogo waliposikia walitoroka, na yule mwanaume pia alitoroka hawakuonekana.

 

Siku moja nilisikia kuna Shirika la Agape lipo linaonesha sinema, nilikwenda kuagalia na nikaomba Mkurugenzi wanirudishe shule. Sasa niko nasoma. Nashukuru Agape sana na MoMEC kwa kunisaidia.