Ushuhuda Jenny

Aliolewa akiwa na miaka 14

Jina langu naitwa Jenny, nilizaliwa mwaka 1998, nilimaliza darasa la saba mwaka 1998 nikiwa na miaka 13. Nilifaulu na nikachaguliwa kwenda kidato cha kwanza.  Lakini sikuweza kwenda maana baba yangu alinikatalia, nilipoanza alinikataza na kuanza kunitukana kwamba hakuna faida ya  ya mtoto wa kike kusoma.

 

Alianza kuleta wanaume nyumbani kuniona ili niolewe, baadae mmoja alikuja alikubaliana na mahari ilijadiliwa.  Alinilazimisha niolewe nikiwa na umri wa miaka 14, mume wangu alikuwa a umri wa miaka 36

 

Nilipofika nyumbani kwa mume wangu, maisha yalikuwa ya mateso makubwa. Alikuwa ananishangaa kwanini niko kwake, akawa ananiuliza kwanini nilikubali kuolewa, alinisimanga na kuniambia ni vizuri nirudi kwetu.  Wakati mwingine nilikuwa namjibu na kumwambia yeye ndie alikuja kwetu kunichumbia na kisha kunioa. Alikataa akasema ni tama ya baba yangu ya kutaka pesa. Mume wangu alikuwa mkatili sana, alikuwa akinipiga sana mara kwa mara.

Nilipata ujauzito, lakini aliedelea kunifanyia ukatili na kunipiga.  Hata hospitali hakuwa ananipeleka nikiumwa. Alisema yeye hahusiki na mimba yangu, mtoto sio wake nitafute baba ya huyo mtoto aliyeko tumboni.  Alianza kusema ataniua, nirudi kwa wazazi wangu. Nilimbembeleza nikae mpaka nitakapojifungua, aliedelea kuwa ananitukana na kunipiga, hasa akirudi amelewa. Hakujali kabisa kwamba nilikuwa mja mzito hata nilipokuwa najisikia kuumwa hakunionea huruma

 

Siku moja alinionesha kisu na kusema ‘nakwenda zangu matembezini kustarehe, nikirudu nisikukute hapa, nitakuua’. Niliamua kwenda kwa wazazi wangu.

Baba yangu hakufurahia kitendo hicho, akasema ni vyema tusuruhishwe nirudi maana alilipa mahari kwa huyu mume na hana kitu cha kurudisha.  Mume wangu aliitwa na akasema kwamba mimi ni muongo na nimetunga maneno ya uzushi.  Akamwambia baba yangu nirudi naye nyumbani, nikakataa. Nilibaki nyumbani nikajifungua na sasa nina mtoto mmoja wa kike.

 

Siku moja watu wa shirika la Agape Aids Control Programme (AACC) walitembelea kijijini kuonesha sinema ya kuelimisha kuhusu madhara ya ndoa za utotoni. Nilihudhuria na nikawaomba nijiunge shule ya Agape nami nisome niweze kufanya mitihani.

 

Baba yangu alikataa, nilimbembeleza na nikaenda kuogea na Mtendaji wa Kijiji ambaye alinisaidia kumuomba baba aniruhusu.  Baba yangu hakutaka kujihusisha kabisa na masuala ya elimu yangu kama kugharamikia vifaa vya shule, unifomu. Alikataa hata kunipa nauli ya kusafiri kwenda shule, maana ilikuwa ni mbali toka kijijini. Ilibidi nidandie magari tu nikawaomba msaada.

Ninashukuru sana AACC na MoMEC kwa kunisaidia kuedelea a masomo

 

Ninaomba wanaume wanaooa watoto wadogo waache.  Ninawaomba wazazi, walezi, kina baba na mama kukomesha hii mila ya kuozesha watoto wadogo.  Tunakutana na matatizo makubwa na tunafanyiwa ukatili.  Tunaomba mtusaidie turudi kusoma.