Mkutano na Waadishi wa Habari Tarehe 9/01/2017 - Shinyanga

FILAMU FUPI YA SAUTI YA KUNESE – SAUTI YA MTOTO MJANE

Habarini za asubuhi mabibi na mabwana waandishi wa habari , karibuni katika mkutano huu wa waandishi wa habari. Tukishirikiana na Agape Aids Control Programme (AGAPE) na Paralegal Aid Centre Shinyanga (PACESHI)

Lengo kuu la mkutano huu ni kuwataarifu kuhusu uzinduzi wa filamu fupi ya SAUTI YA KUNESE (SAUTI YA MTOTO MJANE). Filamu hii inatokana na utafiti uliofanyika mwaka 2003 na ufuatiliaji wake ulikuwa 2015.

Dr Monica Mhoja Edutainment Centre (MOMEC) ni taasisi isiyo ya kiserikali, isiyofungamana na chama chochote, isiyogawana faida inayotumia sanaa kuelimisha kuhusu ukatili wa kijinsia, haki za kisheria na binadamu. Kwa sasa kati ya mikakati yake imejikita katika kutokomeza ndoa za utotoni na madhara yake ikiwemo WATOTO-WAJANE.

DHAMIRA ya MOMEC ni "Kuelimisha, kuhamasisha na kuwajengea uwezo wanawake na wanaume kupinga ukatili wa kijinsia, ukiukwaji wa sheria na haki za binadamu kwa kutumia sanaa zenye kuelimisha na kuburudisha" kupitia filamu ya SAUTI YA KUNESE tuna lengo la kusaidia kuchangia mabadiliko ya fikra na mila zilizopitwa na wakati kuhusu unyanyasaji wa wajane na hususan wajane-watoto. Kwasababu chanzo cha wajane-watoto ni ndoa za utotoni, ni kuhamasisha jamii iondokane na kuwaozesha mabinti wakiwa wadogo bali elimu na usitawi wa maedeleo ya watoto yapewe kipau mbele.

Leo tunataka kujikita zaidi kwa watoto-wajane maana ni suala ambalo halitiliwi manani. Kupitia filamu hii mkakati wetu ni kushirikiana na AGAPE na PACESHI kuibua watoto wajane hapa Shinyanga na Simiyu kuwapa msaada wa sheria na kwa wale walio na ari ya kusoma kuwasaidia kupata wafadhiri na kusoma au kuwajengea uwezo wa kiuchumi kulingana na mahitaji yao. Nanyi waandishi wa habari tunaomba muwe sehemu ya kuibua watoto hao na kuwasiliana nasi. Tutakuwa na utafiti mdogo vijijini mwaka huu kutumia filamu ya SAUTI YA KUNESE kuibua watoto hawa.

Filamu hii inagusia Ndoa za utotoni za kulazimishwa, kutothaminiwa usitawi wa mtoto katika masuala ya elimu, ukatili wa kijinsia kama ukeketaji na unyanyasaji, mfumo dume katika maamuzi, kudhulumiwa mali mjane-mtoto na watoto wake. Sheria za Kimila za Mirathi (Tamko la Serikali 1963)[1] linawaweka watoto hawa katika hali ya kugandamizwa zaidi kwanza kama wajane na pili kama watoto. Hawaruhusiwi kurithi ardhi ya familia au ukoo, lakini sheria hiyo inasema wao wanaweza kurithiwa wakikubali, hawawezi kuwa wasimamizi wa mirathi, wanarithi daraja la tatu.

Sheria ya Kimila inakwenda kinyume na Sheria ya Mtoto (2009) na Sheria za Kimataifa za Haki za Mtoto.

Sehemu ya NANE ya Sheria ya Mtoto inatoa wajibu wa Serikali ya Mtaa kulinda na kuwa na daftari la watoto walioko katika mazingira magumu (hii ni pamoja na watoto-wajane). Wajibu wa kuripoti ukiukwaji wa haki za mtoto katika Sheria ya Mtoto, 2009 -Kifungu95.-(1) Utakuwa ni wajibu wa kila mwanajamii ambaye ana ushahidi au taarifa kwamba haki za mtoto zinakiukwa au mzazi, mlezi na ndugu anayemlea mtoto ana uwezo, lakini hataki kumpatia mtoto chakula, malazi, haki ya kucheza na kufurahi, mavazi, huduma za afya na elimu au kumtelekeza, kuripoti suala hilo kwenye mamlaka ya Serikali za Mitaa ya eneo hilo.

Kila mmoja wetu anaweza kusaidia SAUTI YA KUNESE (MTOTO MJANE) ISIKIKE

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga atazindua filamu ya SAUTI YA KUNESE tarehe 10/01/2017 katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa, Saa Tatu asubuhi.

Filamu itazinduliwa Shinyanga ambako matukio haya yalitokea na Shinyanga inaoongoza kwa ndoa za utotoni kwa takwimu za mwaka 2012. Tanzania imetajwa kuwa ni moja kati ya nchi zenye viwango vya juu vya matukio ya ndoa za utotoni. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti uliochapishwa mnamo Januari, 2016 uliitaja kuwa ni nchi ya tatu barani Afrika kwa matukio ya ndoa na mimba za utotoni kwa 28%.

Takwimu za shirika la Watoto Duniani (UNICEF 2012) lilitaja mikoa inayoongoza kwa ndoa za utotoni huku mkoa wa Shinyanga ukiongoza kwa 59%, ukifuatiwa na Tabora 58%, Mara 55%, Dodoma 51%, Lindi 48%.

Kwasababu chanzo cha watoto wajane ni ndoa za utotoni - MoMEC, AGAPE na PACESHI TUNATOA ombi kwa serikali kupitia wizara na taasisi husika kuongeza kasi kwenye jitihada za kubadili vifungu vya sheria ya ndoa no.5 ya mwaka 1971 vinavyomruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi na miaka 15 kwa ridhaa ya mahakama. SELEMA SELEMA KUKOMESHA NDOA ZA UTOTONI iwe ya mwendo kasi.

Tunatoa wito kwa wabunge wetu kuangalia na kufuta vipengele vinavyokiuka haki za binadamu za wajane katika Sheria za Kimila. Mtoto-mjane anaathirika maradufu.

Filamu hii iliongozwa na Ediga Ngelela wa Keen Insights Production ambaye ni mtaalamu wetu wa sanaa MOMEC akisaidiana na Dr Monica Mhoja (mtaalamu wa masuala ya Sheria na haki za binadamu).

Dr Monica Magoke-Mhoja – MKURUGENZI MoMEC

Consultant

International Human Rights Award Winner (2003) ABA-Litigation Section

Tel: 0788319443

Email: momeccentre@gmail.com

[1] The Local Customary Law (Declaration No.4) Order, 1963, (Government Notice No.436)

Featured Posts
Recent Posts
Archive