Uzinduzi wa Filamu ya Sauti ya Kunese, Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa, Tarehe10.01.2017

Filamu fupi ya SAUTI YA KUNESE inayohusu madhara ya ndoa za utotoni, hususani kufiwa katika umri mdogo ilizunduliwa Shinyanga tarehe 10 Januari 2017. Lengo kubwa ni kuwezesha filamu hiyo kutumika katika kuhamasisha ili kuleta mabadiliko chanya. Uzinduzi huo ulihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo wabunge, madiwani, viongozi wa dini, wanafunzi, wahanga wa ndoa za utotoni na wadau kutoka asasi mbalimbali. Afisa Maendeleo wa Mkoa alizindua kwa niaba ya Mkuu wa mkoa.

Ifuatayo ni hotuba iliyosomwa kwa niaba ya mkuu wa mkoa.

Dr Monica Mhoja –Mkurugenzi MOMEC

Mwl Perpetua Mahudi- Mkurugenzi PACESHI

Nd John Myola –Mkurugenzi AGAPE

Ndg Edgar Ngelela Muongozaji Mkuu (Mkurugenzi Keen Insights Productions)

Wageni waalikwa maalumu

Viongozi wa Serikali mliopo hapa;

Wawakilishi wa Mashirika na Wahisani mbalimbali;

Ndugu Waandishi wa Habari;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana;

Awali ya yote, tuna kila sababu kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa rehema na upendo wake , kwa kutupa uzima na afya kutuwezesha kukusanyika katika uzinduzi huu siku ya leo.

Wageni waalikwa; Mabibi na Mabwana

Napenda nianze moja kwa moja kusema, mimi kama mama, kiongozi wa juu mkoani Shinyanga swala hili husika la ndoa za utotoni linaniumiza sana. Ndoa za utotoni ni ukiukwaji wa haki za binadamu, ni ukatili uliokithiri, na unatakiwa kupigwa vita kwa kila hali. Kutumia sanaa katika kuhamasisha kukomesha ndoa za utotoni ni mkakati mzuri utakaochangia kufikisha habari kwa wengi.

Ofisi ya mkuu wa Mkoa, inaunga mkono asasi mbalimbali zinazojitoa kupigania haki. Mkakati huu uliochokuliwa na MOMEC wa kutengeneza filamu za mafunzo ili kuwafikia Watanzania wengi kuleta mabadiliko ya kifikra kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati ni kitu kinachostahili pongezi na kuungwa mkono. Hongereni sana. Shukrani pia kwa wataalamu kutoka Keen Insights Production katika kufundisha wasanii, Mkurugenzi Edgar Ngelela asante kwa juhudi zako ili waelimishe jamii.

Wageni waalikwa; Mabibi na Mabwana,

Lakini hawakuiishia hapo, wameona wakusanye nguvu kwa kushirikiana na wadau wengine hususani PACESHI NA AGAPE za Shinyanga ili kwa pamoja waweze kumsaidia mtoto kupata haki zake za kisheria, kuhamasisha jamii kujua madhara ya ndoa za utotoni na kumsaidia mtoto huyu kurudi shuleni. MoMEC watakuwa wakitumia sehemu ya faida kusomesha watoto hawa, kama mlivyosikia shuhuda za watoto kutoka Shinyanga na wasanii walivoonesha pia kipande cha yaliyomo kwenye filamu ya SAUTI YA KUNESE.

Wageni Waalikwa; Mabibi na Mabwana;

Nitumie nafasi hii kukupongeza wewe Dr Monica Mhoja na timu yako nzima ya MoMEC kwa kuwa chachu ya kuanzisha umoja wa asasi hizi na kufanya kazi pamoja. Nimedokezwa kuwa filamu nyingi zitazofuata zitatokana na tafiti zilizofanyika kutokana shahada yako ya uzamili na mmeanzia na mkoa wa Shinyanga ambako kunaongoza kwa ndoa na mimba za utotoni. Pongezi kwa John Myola kwa kuanzisha sekondari ya kuweza kuwachukua watoto walioolewa na kuachika, kutekelezwa au kufiwa. Pongezi pia kwa PACESHI kwa kutoa msaada wa sheria

Napenda nipongeze hatua zenu zote hizi, napenda kutumia fursa hii kuwaomba watanzania kina baba waache kuoa watoto wadogo, wazazi waache kuozesha watoto wadogo, mtoto apewe elimu kwanza kwa faida yake na jamii ya Kitanzania kwa ujumla.

Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kuwahakikishia kuwa, mimi binafsi na ofisi ya mkoa, tutakuwa nanyi bega kwa bega katika kila hatua mtakayopiga kuhakikisha kwamba; ndoa za utotoni zinatokomezwa kabisa.

NINATAMKA KWAMBA FILAMU YA KUELIMISHA IITWAYO SAUTI YA KUNESE IMEZINDULIWA LEO RASMI KWA KUKATA UTEPE WA DVD

Mimi nitakuwa wa kwanza kununua DVD hii.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Matukio ya picha mbalimbali wakati wa uzinduzi wa filamu fupi ya SAUTI YA KUNESE

Featured Posts
Recent Posts
Archive